Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Sayansi ya Mkoa wa Lindi katika Kata ya Kilangala umefungua fursa kwa miradi mingine ya Maji, Barabara na Umeme kupelekwa kwa haraka katika Kata hiyo.
Akizungumza katika kikao cha mapokezi ya Timu ya Wataalamu kutoka Benki ya Dunia, Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Juma Mnwele amesema baada ya kuanza kutekeleza mradi huo huduma zingine kwa haraka zikaanza kufika Kilangala eneo ambalo lipo umbali wa Kilomita 50 kutoka Manispaa ya Lindi.
“Tulipopokea fedha kutoka Serikali kuu Tsh Bil. 3 kwa ajili ya ujenzi wa shule na tukasafisha eneo tayari kwa ujenzi Taasisi zingine kama TARURA, RUWASA na TANESCO nao wakaanza kupeleka huduma kwenye Kata ile. Kwa ghafla Kata imebadilika na wanachi wanafurahia maendeleo yaliyopelekwa na Serikali yao,” alisema Mnwele.
Pia aliishukuru Serikali kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (BOOST) kupeleka fedha za kutekeleza miradi hiyo kwani kwa Manispaa kwa awamu ya kwanza wamepokea Shilingi bil. 3 za ujenzi wa shule ya Mkoa na Shilingi mil. 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ijulikanayo kama Zainabu.
Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) nchini kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Robert Msigwa amesema lengo la kutembelea miradi hiyo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi, kushauri na kuona kama miradi hiyo imefuata viwango vya ujenzi vilivyowekwa na Serikali kwa makubaliano na Benki ya Dunia.
Mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na shule itapokea wanafunzi kuanzia Julai, 2023.