PROF. CAROLYNE NOMBO ANENA NA WATUMISHI WA WIZARA KWENYE KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Published on Thursday 20 April, 2023 13:33:12

Wathibiti Ubora wa Shule nchini wametakiwa kuongeza kasi ya ufuatiliaji shule zote za umma na binafsi ili kubaini na kukabiliana na changamoto za unyanyasaji wa wanafunzi hali ambayo inaonekana kukithiri hasa suala la maadili na ukatili wa jinsia kwa wanafunzi.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika uzinduzi wa Mkutano wa 31 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia uliofanyika jijini Arusha.
 
Ameeleza kuwa Wathibiti Ubora wanapaswa kuendelea kupambana na suala hilo na kuwataka kutokulala bali wapambane kuona unyanyasaji wa wanafunzi na mambo  yanayokwenda kinyume na mila na desturi za Kitanzania yanakomeshwa ili kuzuia vitendo hivyo.
 
Aidha, Prof. Nombo amewataka Wajumbe wa mkutano huo kuendelea kuhamasisha umma kupinga vikali masuala ya unyanyasaji wa watoto pamoja na matendo yanayoendelea katika baadhi ya jamii ambayo ni kinyume na mila na utamaduni wa nchi pamoja na ukiukwaji wa miongozo mbalimbali ya elimu hasa suala la kutoa adhabu zilizopitiliza.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa amesema kumekuwa na wimbi la watu katika shule kufundisha watoto wa Kitanzania masuala yaliyo kinyume na desturi, mila na tamaduni za nchi na kuiomba Wizara kuziangalia shule kwa makini zaidi ili kuondoa changamoto hizo.
 
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwa sasa elimu inayotolewa nchini ni bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na ameipongeza Wizara kwa jinsi ambavyo inaendesha zoezi la mabadiliko ya mitaala na mapitio ya Sera ya Elimu ili iweze kuzalisha wahitimu wanaoendana na soko la ajira la kimataifa.
 
Naye Katibu wa Baraza, Huruma Mageni amesema kazi ya Baraza la wafanyakazi ni kuishauri Wizara juu ya utekelezaji wa majukumu yake na kushirikiana na Menejimenti kuhakikisha malengo ya kutoa elimu bora kwa wote yanatimizwa, na kushughulikia masuala yanayohusu Wizara.

Read 524 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top