Jumatatu, 09 Septemba 2019 14:37

SERIKALI YATANGAZA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU VYUO VYA SERIKALI.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza sehemu ya pili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya ualimu katika vyuo 35 vya serikali.

Akitoa taarifa hiyo jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema jumla ya wanafunzi 2,834 wamechaguliwa kujiungana mafunzo ya ualimu ambapo kati yao 1,013 ni wa Astashahada na 1,821 ni wa Stashahada.

Dkt. Akwilapo ameongeza kuwa hadi sasa jumla ya wanafunzi 11,028 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vya serikali ambapo kati yao wanafunzi 8,194 walichaguliwa awali na TAMISEMI na 2,834 wamechaguliwa na NACTE.

Aidha, Dkt. Akwilapo amewataka wanafunzi hao waliochaguliwa kuripoti katika vyuo walivyopangiwa kuanzia tarehe 20 Septemba mwaka huu na kwamba mwisho wa kuripoti ni tarehe 6 Oktoba mwaka huu. Amesisitiza wahakikishe wanaripoti ndani ya muda huo kwani baada ya hapo hawatapokelewa na nafasi zao zitajazwa na wengine wenye sifa ambao walikosa nafasi.

“Wanafunzi wote waliochaguliwa wanatakiwa waripoti katika vyuo vyao kuanzia tarehe 20 mwezi huu hadi 6 Oktoba mwaka huu.  Watakaoripoti baada ya hapo hawatapokelewa na nafasi zao zitajazwa na wanafunzi wengine walioomba ambao wana sifa ila walikosa nafasi,” amesisitiza Dkt. Akwilapo.

Aidha, Dkt. Akwilapo amesema serikali inatambua kuwepo kwa wanafunzi wengi waliokosa nafasi za kujiunga na masomo katika kozi mbalimbali na hivyo ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kufungua dirisha dogo la udahili kwa siku 14 kuanzia tarehe 7 Septemba ili wanafunzi waliokosa nafasi za masomo katika kada mbalimbali waweze kutumia fursa hiyo.

“Wizara inatambua kuwepo kwa idadi kubwa ya waombaji waliokosa nafasi katika awamu hii kutokana aidha na ushindani au kutofanya uchaguzi sahihi wa kozi hivyo wizara inaiagiza NACTE kufungua dirisha dogo la udahili kuanzia leo tarehe 7 hadi 21 Septemba ili kuwapa nafasi waombaji waliokosa nafasi katika programu mbalimbali waweze kufanya uchaguzi upya,” amesema Dkt. Akwilapo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Avemaria Semakafu akiongea katika mkutano huo amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakichagua kozi ambazo hawana sifa zinazohitajika. Amewaasa waombaju kuzingatia sifa za kozi ili kuepuka kuenguliwa kwani masharti yanayowekwa kuhusu sifa hayabadilishwi.

“Utakuta kwa mfano mtu ana ufaulu mzuri wa alama A hadi C katika masomo ya lugha, badala ya kuchagua kozi zinazotaka ufaulu wa lugha yeye atachagua kozi za masomo ya sayansi ambayo kapata alama D, matokeo yake anajikuta hachaguliwi katika kozi alizoomba,” amesema Dkt. Semakafu.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa NACTE, Twaha Twaha amewatahadharisha waombaji hasa wa kozi za afya kuhakikisha kuwa wamefaulu vizuri katika masomo ya sayansi kwani ndio sifa ya msingi katika udahili wa kozi hizo.

“Katika kozi za afya vigezo vinaangalia masomo, mfano mwanafunzi anayetaka kusoma clinical medicine au nursing, anatakiwa awe na ufaulu wa alama D katika masomo ya Physics, Chemistry na Biology. Sifa zote hizi zipo katika kitabu cha Mwongozo wa Udahili ambacho kinapatikana kwenye tovuti ya NACTE ambayo ni www.nacte.go.tz,” amesema Twaha.

Imetolewa na :
Kitengo cha Habari
Wizara ya Elimu, Sayansi na Technolojia.
Read 5098 times

Video News

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: 
  •               Mtaa wa Afya - Mtumba
  •               P.O.Box 10
  •               Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…