WATAALAMU WA SAYANSI WATAKIWA KUSHAURI MATUMIZI YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA MAENDELEO

Published on Wednesday 03 July, 2019 11:23:12

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wanasayansi wanachama wa Akademia ya Sayansi Tanzania (TAAS), kutumia ujuzi wao kutoa ushauri wa matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika shughuli za maendeleo nchini.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la tatu la Akademia hiyo ambapo amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema ustawi wa Baraza hilo ili liweze kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Sayansi, Teknolojia na Ubunifu vinatumika kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu ya uchumi nchini.

“Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 unalenga kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025; Mpango umeeleza bayana kuwa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni nyezo muhimu katika azma hivyo serikali na wataalamu kama ninyi tuna wajibu wa kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika jamii,” alisema Waziri Ndalichako.

Alisema ni vizuri Baraza hilo likajikita katika kukuza na kuendeleza Ubunifu na Ugunduzi wa maarifa ya kisayansi katika nyanja za kijamii na kiuchumi kwa kutoa ushauri na maoni kuhusu Sera na mikakati ya kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za kisayansi zenye kutoa utatuzi wa changamoto katika jamii hasa kipindi hiki dunia inapoelekea katika mapinduzi ya nne ya viwanda.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imechukua hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kufundishia katika ngazi zote za elimu ikiwa ni pamoja na kuzindua Mwongozo wa kutambua na kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa, kuanzisha vituo vya kulea ubunifu na ugunduzi na kwamba itaendelea kushirikiana na Baraza hilo ili kuhakikisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanafanikiwa.

“Utaona katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imewawezesha wabunifu 30 kwa kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 1, hii inatokana na ukweli kwamba inawatambua na ina lengo la kuendeleza kazi zao,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amempongeza Rais Mteule wa Baraza jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania Prof. Yunus mgaya pamoja na mabaraza yaliyotangulia kwa kuendeleza Akademia hiyo iliyoanza rasmi mwaka 2005, kwani wanachama wake wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kujitolea na kwamba anatambua mchango wao katika kukuza na kuendeleza matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Rais huyo mteule wa TAAS Mgaya amesema Akademia hiyo imejipanga kuongeza wanachama na kufanya tafiti, kusaidia wanasayansi kuchapisha tafiti hizo katoka majarida yanayotambulika kimataifa, lakini kubwa zaidi ni kuhuisha matumizi ya Sayansi na teknolojia katika maendeleo ya uchumi.

Baraza la Akademia ya Sayansi Tanzania lina wanachama wanasayansi 131 kutoka nyanja mbalimbali za Sayansi nchini.

Imetolewa na

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

03/07/2019

Read 1771 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top