NDALICHAKO AZINDUA MABARAZA YA UJUZI YA KISEKTA

Published on Friday 21 June, 2019 13:34:58

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu inaendelea kuimarisha stadi na ujuzi katika sekta sita za kipaumbele ili kufikia azma ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa halfa ya uzinduzi wa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta jijini Dar es Salaam ambapo mabaraza hayo yaliyoundwa kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) na sekta zilizopewa kipaumbele katika Mpango Mkakati wa Taifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi ni pamoja na Kilimo, TEHAMA, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na Utalii.

“Katika azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025, tunapaswa kuhakikisha nchi yetu inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi na stadi stahiki zinazohitajika kwenye soko la ajira,” amesisitiza Waziri Ndalichako.

Akizungumzia Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta Prof. Ndalichako amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliingia makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ili kusimamia uanzishaji na kuratibu mabaraza hayo ambayo yatakuwa kiunganishi muhimu kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa masuala ya kuendeleza na kutumia ujuzi nchini.

“Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi na wadau wengine kwa kuweka mifumo wezeshi na rafiki, programu mbalimbali za kuendeleza ujuzi, na kuimarisha miundombinu ili kuhakikisha nchi inajenga ujuzi na stadi stahiki kwa ustawi wa maendeleo ya nchi,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema kupitia ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Umma serikali inatarajia kupata ushirikiano katika programu za mafunzo ya wahitimu tarajali mahali pa kazi (internships) na kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (recognition to prior learning - RPL) ili kupunguza na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

Aidha, Prof. Ndalichako ametoa ombi kwa sekta binafsi kuendelea kupokea vijana wanaokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea utayari wa kuingia kwenye soko la ajira.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte alisema mabaraza yatakuwa ni fursa pekee ya kuunganisha Taasisi Binafsi, Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka nje ya nchi katika kuleta ufanisi katika maendeleo.

Shamte amesema TPSF imekuwa ikitoa ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) katika ngazi ya wilaya, Mkoa , Wizara na hata Taifa ili yaweze kufanyiwa kazi.

Read 1712 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top