| HATUA ZILIZOCHUKULIWA KUTATUA MGOGORO BAINA YA WAMILIKI NA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA TIBA NA TEKNOLOJIA (IMTU) | | Print | |
Mgogoro wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (International Medical and Technological University – IMTU) umedumu kwa miezi 8 sasa tangu ulipoanza mwezi Julai, 2011. Mgogoro huu ulihusu wanafunzi kupinga ada ya Chuo Kikuu hicho kuwa kubwa; ada kulipwa kwa ulinganishi wa thamani ya Dola ya Kimarekani kwa wanafunzi wa Kitanzania; na matatizo ya kitaaluma na kiutawala ya Chuo.Baada ya kufanya vikao mbalimbali vilivyowashirikisha Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Bodi ya Mikopo, Wanafunzi, Uongozi na Mmiliki wa IMTU, Serikali ilitoa tamko tarehe 8/11/2011 kwenye vyombo vya habari kuhusu hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro wa IMTU. 2.0 Maelekezo ya Wizara kwa TCU Baada ya kutoa Tamko hilo, Wizara iliwaandikia TCU barua tarehe 15/11/2011 na tarehe 01/02/2012 kuwaelekeza wafanye yafuatayo: 2.1 TCU ifuatilie kikamilifu utekelezwaji wa Mwongozo wake kwa Vyuo Vikuu vyote nchini unaotaka utozaji na ulipaji wa ada uwe ni kwa kutumia Shilingi ya Tanzania kwa wanafunzi wa Kitanzania. 2.2 TCU ishirikiane na Uongozi wa IMTU katika kufanikisha zoezi la kuwahamisha wanafunzi wa IMTU ambao wanataka kuhamia Vyuo Vikuu vingine ili mradi wanakidhi vigezo na taratibu ziliopo za kuhamia Vyuo Vikuu vingine. 2.3 TCU ifanye ukaguzi wa kitaaluma na kiutawala kwenye Chuo Kikuu cha IMTU ili kubaini ukweli wa malalamiko ya wanafunzi na kupendekeza hatua za kuchukua. 3.0 Hatua Zilizochukuliwa na TCU 3.1 TCU imeshirikiana na Uongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha IMTU pamoja na Vyuo Vikuu katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Tarehe 11/1/2012, TCU ilikutana na mwakilishi wa Mmiliki wa IMTU na Uongozi wa wanafunzi wa IMTU. Makubaliano ya kikao hicho yalitangazwa kwenye vyombo vya habari tarehe 23/1/2012. Aidha, tarehe 14/2/2012 TCU iliwasilisha Wizarani ripoti ambayo ilikuwa inaelezea hatua zilizochukuliwa na TCU katika kutekeleza maagizo ya Serikali. 3.2 Kutokana na maamuzi ya kikao cha tarehe 11/1/2012, Uongozi wa IMTU umekubali kutoza ada kwa kutumia Shilingi ya Tanzania kuanzia mwaka wa masomo 2011/12. Pia wanafunzi wa Tanzania watatozwa ada ya Shilingi 6,250,000/= kwa mwaka mpaka hapo ripoti ya ‘Gharama Halisi ya Mwanafunzi’ (Student Unit Cost)” itakapotolewa na Serikali. Kwa kutotoza ada kwa ulinganishi wa Dola ya Kimarekani, ina maana kuwa tatizo la ada ya IMTU kupanda kila mwaka kulingana na thamani ya Dola litakuwa limekwisha. 3.3 Ili kusimamia zoezi la wanafunzi wa IMTU kuhamia Vyuo vingine, TCU iliandika barua kwa Vyuo Vikuu vyote saba vya udaktari nchini kuwaomba waangalie uwezekano wa kuwapokea wanafunzi wa IMTU wanaotaka kuhamia kwenye Vyuo vyao. Vyuo Vikuu hivyo vilitakiwa vijiridhishe kuwa vigezo na taratibu zote za kuhama zinafuatwa. Wanafunzi 433 wa IMTU walioomba kuhamia vyuo vikuu vingine na mchanganuo wa uhamisho wa wanafunzi hao ni kama ifuatavyo:
Baadhi ya wanafunzi wameshindwa kuhamia Vyuo Vikuu vingine kutokana na Vyuo Vikuu hivyo kutokuwa na nafasi au kutokuwa na programu zinazofanana moja kwa moja na zile za IMTU au wanafunzi kutokidhi vigezo na masharti yaliyopo ya kutaka kudahiliwa au kuhamia kwenye Vyuo Vikuu hivyo. 3.4 Kufanya uchunguzi wa kitaaluma na kiutawala katika Chuo Kikuu cha IMTU ili kubainisha ukweli wa shutuma zilizotolewa na wanafunzi. TCU iliunda Kamati Maalum ya uchunguzi tarehe 19/11/2011 na kumaliza uchunguzi wake tarehe 22/11/2011. Ripoti ya Kamati hii iko katika hatua za mwisho za kukamilishwa na mapendekezo yatawasilishwa Serikalini kwa hatua mbalimbali kwa mujibu wa taratibu na Sheria. 4.0 Maagizo ya Wizara Baada ya majadiliano yaliyofanyika katika mikutano kadhaa ya pande zote zinazohusika na kwa kuwa baadhi ya matatizo ambayo yalikuwa chimbuko la mgogoro yameshatatuliwa kwa kiasi kikubwa na mengine yanaendelea kutatuliwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaagiza yafuatayo yatekelezwe: 4.1 Wanafunzi 25 wa IMTU waliokubaliwa St. Johns bila masharti waripoti chuoni kufuatana na maelekezo waliyopewa. 4.2 Wanafunzi wote 168 waliokubaliwa katika Vyuo Vikuu vingine kwa masharti, wanashauriwa watimize masharti hayo na wajiunge na Vyuo Vikuu hivyo vilivyowakubali. 4.3 Wanafunzi 103 ambao wamerejea IMTU waendelee na masomo yao kwa amani, utulivu na nidhamu. 4.4 Wanafunzi wote 137 ambao hawakupokelewa na Vyuo Vikuu vingine wanashauriwa wakubali kurudi IMTU ili waendelee na masomo yao. 4.5 Uongozi wa IMTU uandae utaratibu wa kuwapokea wanaorudi Chuoni kwa kuzingatia haki, sheria na taratibu za Chuo. 4.6 Chuo cha IMTU kiendelee kutoza ada iliyokubalika na wanafunzi waruhusiwe kulipa ada hiyo kwa mikupuo minne katika mwaka wa masomo. 4.7 Wamiliki wa Chuo, kwa nia njema, waweke mazingira mazuri ya ushirikiano na kuanza ukurasa mpya na kusahau yaliyopita ili kuleta tija katika masomo. 4.8 Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ifanye mawasiliano na Vyuo Vikuu vilivyowakubali wanafunzi kwa masharti kama vile St. Francis (SFUCAS), KCM College na HKMU ili kuharakisha taratibu za kuwasajili. 5.0 MWISHO Kutokana na hatua iliyofikiwa katika mkutano wa tarehe 28/2/2012 kati ya Wizara, Tume ya Vyuo Vikuu, Uongozi wa Chuo cha IMTU na wakilishi wa wanafunzi wa Chuo cha IMTU kuhusu mgogoro huu, Wizara inatoa rai kwa wahusika wa pande zote mbili yaani Wamiliki/Uongozi wa Chuo cha IMTU na Wanafunzi kufanikisha utekelezaji wa makubaliano haya ili kurejesha amani katika Chuo cha IMTU, na hivyo suala hili sasa limefungwa. IMETOLEWA NA: MHE. DKT. SHUKURU JUMANNE KAWAMBWA (MB) WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI 1/3/2012 |