| HATMA YA WANAFUNZI WALIOFUTIWA MATOKEO YA MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI MWAKA 2011 | | Print | |
|
(i) Watahiniwa 94 walikamatwa na ama karatasi au rula au viatu vilivyoandikwa herufi zenye majibu; (ii) Watahiniwa wanne (4) walibainika kuandikiwa majibu; (iii) Watahiniwa tisa (9) walibainika kukariri darasa kinyume na utaratibu; na (iv) Watahiniwa 9,629 walibainika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida.
Baraza la Mitihani la Tanzania liliwafutia matokeo watahiniwa hao 9,736 kwa mujibu wa kanuni za mitihani za mwaka 1984 na rekebisho lake la mwaka 2006, Kifungu Na. 52(b).
Utaratibu wa kufuta matokeo kwa wanafunzi wanaobainika kufanya udanganyifu katika mitihani unalenga yafuatayo:- (i) Kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa watahiniwa wote ili wale wanaofaulu wawe wamefaulu kihalali; (ii) Kujenga maadili miongoni mwa wanafunzi kwa kuamini kuwa udanyanyifu katika elimu ni suala lisilokubalika; na (iii) Kujenga dhana ya kujiamini na kujitegemea miongoni mwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Kufuatia uamuzi wa kufuta matokeo ya mtihani kwa wanafunzi hao 9,736, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekuwa ikipata malalamiko na maoni mbalimbali kutoka kwa wazazi, walezi, jamii na wadau wengine wa elimu kuhusu hatua zilizochukuliwa na athari zake kwa wanafunzi waliofutiwa matokeo hayo. Baada ya kutafakari suala hili kwa kina Serikali imeamua kuchukua hatua zifuatazo:- (i) Kuwaruhusu watahiniwa 9,629 waliofutiwa matokeo kutokana na kubainika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida kurudia Mtihani huo wakati wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwezi Septemba mwaka huu 2012 utakapofanyika. Halmashauri kwa kushirikiana na shule ziandae utaratibu utakao wawezesha watahiniwa hao kutotoka nje ya mfumo wa elimu mpaka watakapofanya mtihani huo. Serikali inapenda kusisitiza kuwa ruhusa ya kurudia mtihani imetolewa mwaka huu tu. Watahiniwa 107 waliofutiwa matokeo ya mtihani kwa kukutwa na majibu, waliokariri darasa na walioandikiwa majibu hawatahusika na uamuzi huu;
(ii) Wanafunzi waliofutiwa matokeo na watakaorudia mtihani mwaka 2012 watapaswa kusajiliwa kwa ajili ya mtihani ili taarifa zao zifike Baraza la Mitihani la Tanzania kabla ya tarehe 30/01/2012;
(iii) Kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha udanganyifu huo na kutoa mapendekezo ya kudhibiti udanganyifu katika mtihani. Taarifa ya uchunguzi huo itatolewa mwishoni mwa mwezi Aprili 2012. Pamoja na hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na mamlaka mbalimbali, watendaji na au taasisi zitakazobainika kuhusika kwa namna yoyote ile na udanganyifu huo zitachukuliwa hatua zinazostahili.
Napenda kutumia fursa hii kuwatanabahisha tena wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kwamba jukumu la utoaji, usimamizi na uendeshaji wa elimu ni letu sote. Hivyo, ninawaasa wadau wote na jamii kwa ujumla kujiepusha na udanganyifu katika mitihani na kuwalea watoto wetu katika misingi ya maadili mema, kujiamini na kujitegemea katika maisha yao yote. Suala la udanganyifu katika elimu litalifikisha Taifa hili mahali pabaya sana.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa upande wake haitosita kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika pindi itakapobaini suala la udanganyifu katika elimu.
Hivyo, kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo ili taifa lisonge mbele katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wote ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu bora kwa wote.
Elimu bila udanganyifu inawezekana.
Imetolewa na Dkt. Shukuru J. Kawambwa (Mb) WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
|