WAZIRI NDALICHAKO ASISITIZA USIMAMIZI WA MTAALA SEKTA YA ELIMU MSINGI

Published on Thursday 03 June, 2021 07:53:33

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesisitiza Maafisa Elimu Mikoa, Wilaya na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa Mtaala unaotumika kufundishia Elimu Msingi Nchini ili kukidhi mahitaji.

Mhe. Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo Juni 03, 2021 Mjini Bagamoyo wakati akifungua mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Maafisa Elimu Mikoa, Wilaya na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) katika Kampasi yake ya Bagamoyo yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani katika maeneo yao.

“Ubora wa Mtaala, unaendana na Usimamizi, nendeni mkasimamie vizuri mtaala unaotumika sasa kufundishia elimu ya Msingi Nchini, fanyeni ufuatiliaji wa namna walimu wanafundisha mashuleni, angalieni kama wanafundisha kwa kufuata mtaala wetu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji yatakayotoa wahitimu wenye maarifa na ujuzi wa kutosha” Amesema Profesa Ndalichako

Amesema mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani waliyopatiwa, yawe chachu ya ya kwenda kufanya mabadiliko katika Sekta ya Elimu Msingi Nchini kwa kuhakikisha yanawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi kwa kujifunza kutoa takwimu sahihi na za kweli zinazohusiana na Sekta ya elimu ili Wizara ijue namna bora ya kutatua changamoto za Kisekta katika maeneo yao na kuacha tabia ya kutoa takwimu za uongo kwa kuogopa kuonekana wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

Waziri Ndalichako pia amesisitiza usimamizi mzuri katika Fedha za uboreshaji wa Miundo mbinu ya elimu zinazotumwa katika kila Halmashauri na kuwataka Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, ili lengo la Serikali la kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji liweze kufikiwa. 

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza katika hafla hiyo ya Ufunguzi wa mafunzo hayo amesema, tayari ADEM imeendesha mafunzo hayo kwa kundi la Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 8799 Nchi nzima hadi sasa, Maafisa Elimu Taaluma wa Halmashauri 184, na Wathibiti Ubora wa Shule wa Wilaya 183 na sasa wanaendesha mafunzo hayo kwa kundi la Maafisa Elimu Mikoa, Halmasahuri na Maafisa Elimu Taaluma wa Mikoa wapatao 232 sawa na Asilimia 98 ya washiriki wote waliotarajiwa kuhudhuria mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa GPE – LANES II.

Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Maafisa Elimu Mikoa, Wilaya na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa yanafanyika kwa siku 04 kuanzia tarehe 01 – 04 Juni, 2021 yakilenga kuimarisha eneo la Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani ili kuchagiza uboreshaji wa Sekta ya Elimu Msingi Nchini katika eneo la Ubora wa Mtaala katika kukidhi mahitaji, Uthibiti Ubora wa Shule, Ubora wa ujifunzaji na upimaji mzuri, Mafanikio ya mwanafunzi, Ubora wa Utawala katika Uongozi wa Shule, Ubora wa Mazingira katika kuboresha Ustawi,  Kushirikiana na jamii ili kupata Shule bora na Ufuatiliaji na Tathmini ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani.

Read 602 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top