Wafanyakazi Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia Fanyeni kazi kwa Weledi - Prof. Mdoe

Published on Thursday 16 September, 2021 08:05:44

Watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, kuwa na maadili na kujituma ili kuweza kujenga Taifa lililo bora.

Hayo yamesemwa leo 16 Septemba, 2021 Jijini Mbeya na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. James Mdoe wakati akifungua Mkutano wa 29 wa Baraza la Wafanyakazi ambapo amesema jukumu la Baraza hilo ni kuishauri Wizara juu ya namna bora ya kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa Wizara.

Amefafanua kuwa Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu katika kuushauri Uongozi wa Wizara kuhusu utendaji ulio bora wa kutekeleza majukumu kwa lengo la kuweka mikakati ya kutoa elimu bora pamoja na mikakati  endelevu ya kuendeleza masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

"Watumishi wasiotekeleza wajibu wao na kusimamia maadili na uwajibikaji katika sehemu zao za kazi hawana nafasi katika Wizara hii, wakiwemo wenye lugha zisizofaa, dharau na kutoheshimu muda. Hivyo naendelea kuwasisitiza kutekeleza wajibu wenu na kuwa na maadili pamoja na kujituma ipasavyo ili tujenge Taifa lililo bora," amesisitiza Prof. Mdoe.

Aidha, Prof. Mdoe ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza watumishi kuzingatia kanuni za afya zilizowekwa ili kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19.

"Tuna wajibu wa kuhakikisha tunazingatia kanuni za afya zilizowekwa dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 katika sehemu zetu za kazi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa kwa ufasaha, kutumia vipukusi na kuzingatia social distance," amesisitiza Prof. Mdoe.

Akiongea katika Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu katika kutoa mwelekeo wa utendaji kazi wa Wizara na ni njia ya ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi na mipango ya maendeleo na ustawi wa Wizara.

"Tutambue kuwa sisi wajumbe tuliopo hapa  ni wawakilishi wa wenzetu kwahiyo naamini yatakayojadiliwa hapa yatabeba taswira ya uwakilishi wa wengine walio nyuma yetu hivyo tutoe mawazo ya kuboresha ufanisi na ustawi wa Wizara yetu," amesema Prof. Nombo.

Mkutano huu una kaulimbiu isemayo 'Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kichocheo cha uwekezaji.'

Read 156 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top