VETA ANZISHENI PROGRAMU ZAIDI MAFUNZO YA UVUVI KANDA YA ZIWA- PROF NDALICHAKO

Published on Thursday 27 May, 2021 23:40:28

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Balozi wa China Nchini Tanzania, Wang Ke Mei 25, 2021 wamekabidhi vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa Uongozi wa VETA, vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 350.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Jijini Dar es Salaam ambapo Profesa Ndalichako ameishukuru Serikali ya Watu wa China kwa misaada mbalimbali ikiwemo ufadhili wa Ujenzi wa Chuo cha Kisasa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Mkoani Kagera .

"Kwa niaba ya Serikali naendelea kushukuru Serikali ya Watu wa China kwa misaada mbalimbali wanayoitoa, kipekee ujenzi wa Chuo kikubwa cha kisasa cha VETA Kagera kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi Billioni 22.4," amesema Ndalichako.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kozi za uvuvi na uchakataji mazao ya uvuvi, programu ambayo inatolewa kwa mara ya kwanza na VETA katika Chuo chake cha Chato.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu amesema vifaa hivyo vya kisasa na vyenye ubora ni pamoja na Boti ya uvuvi na vifaa vyake, mashine mbalimbali za kuongeza thamani mazao ya uvuvi yakiwemo majokofu na majiko. 

Msaada huo umekuja ikiwa ni utekelezaji ahadi ya  Serikali ya Watu wa China kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Mhe. Wang Yi alipotembelea na kupata Heshima ya kuzindua Chuo cha VETA Chato.

Aidha, Mhe. Ndalichako ameutaka Uongozi wa VETA kusimamia vema matumizi ya vifaa hivyo na kuwaagiza kuanzisha programu za uvuvi  katika vyuo vyake vyote vilivyopo maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

Naye Balozi Wang Ke ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania  katika kuimarisha mafunzo yanayojenga ujuzi kwa vijana wa Kitanzania kupitia VETA.

Read 559 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top