SHULE ZOTE NCHINI ZAAGIZWA KUTENGA MAENEO MAALUM KWA AJILI YA MICHEZO NA SANAA

Published on Tuesday 22 June, 2021 08:39:44

Serikali imeziagiza shule zote nchini  kutenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo na sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo wakati akifungua mashindano ya 41 ya UMISSETA mjini Mtwara, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, ambapo amesema Wizara ya Elimu itahakikisha kila shule zinakuwa na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya michezo ikiwemo michezo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Amesema Wizara itaboresha ufundishaji wa michezo kama vitalu vya vipaji na msingi wa ushiriki endelevu katika michezo kwa afya, elimu, uchumi na ajira.

"Serikali imejizatiti kuendeleza vipaji vya wanafunzi kupitia kufundisha somo la haiba na michezo kwa shule za Msingi, na Elimu kwa Michezo kwa vyuo vya ualimu, pia kupitia wathibiti Ubora wa Shule itahakikisha kunafanyika tathmini na ushauri wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi" amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Naye Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo amesema michezo yote iliyoshindaniwa wakati wa mashindano ya UMITASHUMTA itakuwepo kwenyeUMISSETA isipokuwa mchezo wa mpira wa goli ambao haujaanza kushindaniwa katika shule za sekondari.

Michezo itakayoshindaniwa katika UMISSETA ni pamoja na mchezo wa soka wavulana, na wasichana, netiboli, mpira wa mikono wavulana na wasichana, mpira wa wavu wavulana na wasichana, riadha wavulana na wasichana, mpira wa kikapu, na kwaya na ngoma katika sanaa za maonesho.

Jumla ya wanafunzi 3200 kutoka mikoa 28 ya Tanzania ikiwemo mikoa miwili ya Tanzania visiwani wanashiriki mashindano hayo ambayo yatafanyika kwa siku 11 katika viwanja vya shule ya Ufundi na Chuo cha Ualimu Mtwara.

Read 746 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top