NDALICHAKO ATAKA USHIRIKIANO SEKTA ZA ELIMU NA BINAFSI

Published on Wednesday 02 June, 2021 23:34:48

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa waajiri na wadau wote ya elimu kushirikiana kwa karibu na vyuo vya mafunzo ili kuvisaidia katika kuvijengea uwezo kuviwezesha kuandaa wahitimu wanaohitajika katika soko la ajira.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo Jijini Dodoma wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi ambapo amesema kuwepo kwa ushirikiano huo kutaondoa changamoto kubwa wanayokutana nayo wamiliki wa vyuo ya kupata sehemu ya kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

“Baadhi ya waajiri wamekuwa na mtazamo hasi na kukataa kuwapokea wanafunzi kwa madai kuwa wanawapotezea muda kwa sababu wanaona kama bado hawajaiva, napenda kuwasihi muone umuhimu wa kuwapatia wanafunzi nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo ili kuwafanyia tathimini kabla hawajamaliza mafunzo,” amesema Prof. Ndalichako.

Amesema kupitia fursa ambazo zitolewa na waajiri kama kutakuwa na mapungufu kwa wanafunzi wanaporudi vyuoni kabla ya kumaliza mafunzo yao vyuo vitachukua hatua za kurekebisha na italeta manufaa zaidi kwa waajiri kwani watapata watumishi walioiva.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Francis Nanai amesema sekta binafsi imekuwa ikitoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na itaendelea kupokea vijana wengi zaidi wa kujifunza kwa vitendo.

Aidha, Nanai ameiomba Serikali kuanzisha chombo cha juu cha kuratibu suala zima la kukuza na kuendeleza ujuzi nchini pamoja na kulinda maslahi ya Taifa na ajira za vijana wa Kitanzania na kuangalia upya masharti ya vibali vya ajira za kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Prof. John Kondoro amesema kufanyika kwa maonesho haya kunasaidia kuchochea ustawi wa sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi nchini na yamewezesha wananchi kuona mchango mkubwa unaotolewa na vyuo vya ufundi katika kuandaa rasilimaliwatu itakayotumika katika ujenzi wa uchumi wa viwanda

Maonesho ya Pili ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi yamefanyika Jijini Dodoma kuanzia Mei 27 hadi Juni 2, 2021 na yameshirikisha Taasisi 151.  Kauli mbiu ya Maonesho hayo ni “Kuimarisha Ushirikiano na Wadau katika Kukuza ujuzi kwa Maendeleo ya Viwanda.”

Read 654 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top