Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea taarifa ya kuwepo kwa kikundi cha watu wanaojitangaza kutoa nafasi za udhamini wa masomo kwa kutumia majina ya ofisi za kibalozi. kikundi hicho kimekuwa kikiwataka waombaji kulipa ada ya maombi kiasi cha shilingi laki sita (600,000/=) za kitanzania.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutaarifu Umma kuwa Wizara haihusiki na kikundi hicho na kwamba watu hao wanafanya shughuli hizo kinyume na taratibu za Serikali. Wizara inapenda kuwajulisha watanzania wote kuwa nafasi zote za masomo zinazotangazwa na Serikali hutolewa kupitia Vyombo mbalimbali vya habari, Tovuti ya Wizara pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu. Watanzania wanaoomba kunufaika na nafasi zinazotolewa na nchi wahisani hawatakiwi kulipa malipo yoyote. Wizara inatoa wito kwa wananchi na wadau wote wa Elimu kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohuska wanapoombwa fedha kutoka kwa wahalifu hao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.
13 Oktoba, 2017